Wanachama wa Baraza la Usalama waikosoa vikali Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57430-wanachama_wa_baraza_la_usalama_waikosoa_vikali_marekani
Rais Donald Trump wa Marekani amechukua msimamo wa kuunga mkono kwa hali na mali na bila ya masharti yoyote utawala haramu wa Israel na licha ya maazimio kadhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanayopiga marufuku kuunganishwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo tokea mwaka 1967, ikiwemo miinuka ya Golan ya Syria, lakini bado serikali ya Washington inauchukulia ukaliaji mabavu huo wa utawala wa Kizayuni kuwa ni jambo halali na linaloruhusiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 22, 2019 23:08 UTC
  • Wanachama wa Baraza la Usalama waikosoa vikali Marekani

Rais Donald Trump wa Marekani amechukua msimamo wa kuunga mkono kwa hali na mali na bila ya masharti yoyote utawala haramu wa Israel na licha ya maazimio kadhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanayopiga marufuku kuunganishwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo tokea mwaka 1967, ikiwemo miinuka ya Golan ya Syria, lakini bado serikali ya Washington inauchukulia ukaliaji mabavu huo wa utawala wa Kizayuni kuwa ni jambo halali na linaloruhusiwa.

Pamoja na hayo lakini hatua ya hivi karibuni ya Marekani kuunga mkono ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaotekelezwa na utawala ghasibu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan imekabiliwa na malalamiko na ukosoaji mkali wa jamii ya kimataifa. Katika uwanja huo siku ya Jumatano tarehe 20 Novemba, wanachama 14 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walikosoa hatua ya Marekani kuhalalisha ujenzi huo wa vitongoji unaofanywa na utawala wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Taarifa iliyotolewa na wanachama hao wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, inalaani ujenzi huo wa vitongoji na kusema kuwa unakiuka wazi sheria za kimataifa. Taarifa hiyo bila shaka inaonyesha wazi kwamba jamii ya Kimataifa, kinyume na matakwa ya Marekani, inapinga hatua hiyo ya utawala haramu wa Israel kuvunja sheria za kimataifa bila kujali lolote. Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia siku ya Jumanne alitoa radiamali yake kuhusiana na siasa hizo mpya za Marekani kuhusiana na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na  kusema kwamba Umoja huo unauchukulia ujenzi huo wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kuwa unakiuka sheria za kimataifa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Marekani imekuwa ikitumia vibaya nafasi yake ya kuwa nchi inayotoa mchango mkubwa zaidi wa kifedha kwa Umoja wa Mataifa kama chombo cha kutoa mashinikizo dhidi ya umoja huo na hasa taasisi zake muhimu kama Baraza la Usalama, ili zikubaliane na matakwa yake ya kijuba. Taasisi hizo zinapokataa matakwa hayo, Marekani huamua kujitoa katika taasisi hizo kama mwanachama, kama tulivyoona ikifanya hivi karibuni katika taasisi muhimu za umoja huo, yaani Baraza la Haki za Binadamu na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO. Pamoja na hayo msimamo wa pamoja uliochukuliwa hivi karibuni na wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wakiwemo washirika wote wa Ulaya wa Marekani, unathibitisha wazi kwamba nguvu laini ya Washington inaendelea kudhoofika duniani siku baada ya nyingine. Kuhusu hilo, Karen Elizabeth Pierce, Mwakilishi wa Kudumu wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa amesema: Shughuli zote za ujenzi wa vitongoji si halali kwa mujibu wa sheria za kimataifa, na bila shaka unaondoa uwezekano wa kutatuliwa mzozo wa Palestina kwa msingi wa kubuniwa nchi mbili na kupatikana amani ya kudumu kama ilivyoainishwa katika azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mike Pompeo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani siku ya Jumatatu tarehe 18 Novemba kwa mara nyingine alitangaza wazi uungaji mkono wa nchi hiyo kwa ukaliaji mabavu wa ardhi za Wapalestina unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel na kuongeza kuwa tokea sasa Washington haitatambua tena ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu katika Ukingi wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. Huku akisisitiza kuwa Marekani imebadili siasa zake kuhusiana na hatua ya Israel kuendelea kujenga vitongoji hivyo katika Ukongo wa Magharibi wa Mto Jordan, Pompeo ametoa matamshi ya kushangaza kwa kudai kuwa ujenzi wa vitongoji hivyo haukiuki sheria za kimataifa.

Karen Elizabeth Pierce, Mwakilishi wa Kudumu wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa

Utawala wa kibaguzi wa Israel inaendelea kupuuza matakwa ya jamii ya kimataifa kwa kuendelea kujenga vitongoji hivyo katika ardhi za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu na hilo linatokana na uungaji mkono mkubwa wa Marekani kwa utawala huo. Ujenzi wa vitongoji hivyo ni haramu kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Umoja wa Mataifa umetangaza wazi msimamo wake kuhusiana na suala hilo. Nikolai Mladinov, Mtartibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Mwenendo wa Amani wa Asia Magharibi, alibainisha wazi masikitiko yake katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na uamuzi wa Marekani wa kuhalalisha ujenzi wa vitongoji vya Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, akisema kuwa huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio nambari 2334 tarehe 23 mwezi Disemba 2016 likiutaka utawala haramu wa Israel usimamishe mara moja shughuli zote za ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Wapalestina unazozikalia kwa mabavu. Pamoja na hayo, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala huo, huku akipata ushirikiano na uungaji mkono wa pande zote wa Marekani, amepuuza azimio hilo na maazimio mengine mengi ya baraza hilo, na kuendelea kujenga vitongoji hivyo, bali hata kuanzisha ujenzi wa vitongoji vingine vipya kwa makusudio ya kuviunganisha na vitongoji vingine vilivyojengwa katika ardhi nyingine za Wapalestina zilizoghusubiwa zamani. Ni wazi kuwa hatua hizo za utawala ghasibu wa Israel zimeupelekea kuendelea kutengwa na jamii ya kimataifa na pia Marekani kutengwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na  uungaji mkono wake wa pande zote kwa hatua zisizo za kisheria za utawala huo.