Tahadhari ya Russia kuhusiana na kuutumia kisiasa mgogoro wa corona
(last modified Fri, 17 Apr 2020 04:23:15 GMT )
Apr 17, 2020 04:23 UTC
  • Tahadhari ya Russia kuhusiana na kuutumia kisiasa mgogoro wa corona

Katika kipindi hiki cha mgogoro wa mlipuko wa virusi vya corona, Marekani ambayo ni kinara wa nchi za Magharibi imeendeleza siasa zake zisizo za kibinadamu dhidi ya nchi hasimu na wapinzani wake, hususn katika kuzidisha vikwazo vya kiuchumi na kuzizuia kupata misaada ya kimataifa. Suala hili limekosolewa sana na madola mengine makubwa duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amewaasa maafisa wa serikali ya Marekani kuacha kuutumia kisiasa mgogoro wa virusi vya corona dhidi ya nchi nyingine. Lavrov amepinga tuhuma za Marekani dhidi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na kusema: "Shirika hili limetekeleza majukumu yake kiufundi, na Moscow inazitaka nchi zote ziache kutumia kisiasa suala la maambukizi ya virusi vya corona. Vilevile nakumbusha kuwa, nafasi nyingi za shirika hili la WHO zinashikwa na wamarekani."

Sergey Lavrov

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alikuwa akiashiria hujuma kali ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya shirika la Afya Duniani na hatua ya kiongozi huyo ya kukata mchango wa kifedha serikali ya Washington kwa shirika hilo la kimataifa. Kwa kutilia maanani kwamba WHO imepongeza hatua zilizochukuliwa na China kupambana na maambukizi ya virusi vya corona, na wakati huo huo imepinga mitazamo ya Trump katika uwanja huo hususan suala la kuondolewa haraka karantini, na imemtahadharisha Rais huyo wa Marekani kuhusu suala la kuanzisha haraka shughuli na kazi za kiuchumi kabla ya maambukizi ya virusi vya corona nchini Marekani hayajadhibitiwa kikamilifu, msimamo huo wa WHO umemkasirisha sana Donald Trump. Rais huyo wa Marekani daima ameonyesha kuwa havumilii wala kukubali kukosolewa na wala hakubaliani na taasisi za kimataifa. Trump ambaye ameiondoa Marekani katika shirika la UNESCO na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, sasa amesitisha mchango wa nchi hiyo katika Shirika la Afya Duniani na anashinikiza Mkurugenzi wake Mkuu ajiuzulu. Ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Shirila la Afya Duniani (WHO) limefanya kosa kubwa. Kutokana na sababu kadhaa, shirika hili linafadhiliwa zaidi na Marekani, lakini wakati huo huo linaipendelea China." 

Madai hayo ya Trumo yamepingwa hata na viongozi wa ndani ya Marekani kwenyewe. Mwenyekiti wa Kamati ya Upelelezi ya Kongresi ya Marekani, Adam Schiff amejibu madai ya Trump dhidi ya WHO akisema: Kama kawaida yake, Donald Trump anataka kuzipotosha fikra za Wamarekani kuhusiana na kufeli kwake (katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona).

Adam Schiff akikosoa sera za Trump

Serikari ya Donald Trump imechukua msimamo huo dhidi ya WHO wakati huu ambapo dunia inalazmika kufuata sera na siasa za aina moja na zinazooana katika masuala ya afya na tiba kwa jili ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona na hapana shaka kuwa, Shirika la Afya Duniani ndilo lenye jukumu la kusimamia shughuli hiyo.

Kadhia nyingine iliyojitokeza zaidi katika kipindi hiki cha janga la corona ni mwenendo wa Marekani wa kukataa kubadili sera zake za kihasama na kiadui dhidi ya nchi zisizokubaliana na siasa za nchi hiyo au nchi wapinzani wake, na mfano wa wazi zaidi wa mwenendo huo wa kikatili wa serikali ya Washington ni kuzidisha vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov amesema: Si jambo sahihi kuziwekea vikwazo vya upande mmoja nchi nyingine hususan katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya corona. Katika kipindi hiki nyeti cha mlipuko wa virusi vya corona duniani, serikali ya Donald Trump imeendelea kuweka vikwazo vya aina mbalimbali dhidi ya Iran. Uadui na uhasama huo wa Marekani umeenda mbali zaidi kiasi cha kuzuia zana na vifaa vya tiba vinavyohitajika kwa ajili ya kupambana na maambukizi ya corona kuingizwa nchini Iran. Washington pia imekwamisha hata juhudi za Jamhuri ya Kiislamu za kupata mkopo wa kisheria wa jumuiya za kimataifa kama Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na corona. Katika uwanja huu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amepuuza ukosoaji mkubwa wa kimataifa dhidi ya mienendo ya serikali ya Washington na pingamizi lake la kuzuia Iran isipewe mkopo wa IMF kwa ajili ya kujiimarisha zaidi katika mapambano yake na janga la corona na kuandika bila kuona haya kwenye mtandao wa Twitter kwamba: “Kinachojiri Iran ni maafa makubwa. Badala ya kuwekeza katika sekta ya afya, Iran inatumia fedha zake katika kufadhili makundi ya kigaidi duniani!”

Mike Pompeo

Haya yote yanajiri katika kipindi ambacho pingamizi na vikwazo vya Marekani vinaendelea kuzuia au kutatiza utumaji wa shehena za misaada na vifaa vya tiba nchini Iran.

Sasa na kwa kutilia maana pingamizi la Marekani dhidi ya kutolewa mkopo wa IMF kwa Iran, msimamo wa shirika hilo la kimataifa kuhusiana na kadhia hii unaweza kuwa kigezo kizuri cha kutathmini madai yake kwamba linataka kuisaidia Iran kupambana na maambukizi ya corona, na vilevile kupima ni kwa kiwango gani IMF inafanya kazi kwa kujitegemea.   

Tags