Jitihada za Macron za kuhalalisha muswada dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa
Hujuma na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya viliongezeka sana baada ya matukio ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani; na mashambulizi ya kundi la kigaidi na lenye misimamo mikali la Daesh katika baadhi ya nchi za Ulaya kama Ufaransa na Uingereza yamezidisha chuki na uhasama dhidi ya Waislamu. Hivi sasa serikali ya Ufaransa ina mpango wa kupasisha sheria ya kuimarisha hujuma na vita dhidi ya Uislamu.
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa Juzi Ijumaa alitoa matamshi yaliyohujumu dini ya Uislamu akihalalisha mpango huo wa serikali yake wa kutaka kupasisha sheria dhidi ya dini hiyo. Macron alizindua muswada wa sheria hiyo na kudai kuwa anataka kukabiliana na kile alichokitaja kuwa ni "misimamo mikali ya Kiislamu" nchini Ufaransa. Rais wa Ufaransa alidai kuwa: "Uislamu ni dini ambayo hii leo imekumbwa na mgogoro kote ulimwenguni." Aliongeza kusema kuwa: "Usekulari ndio nguzo ya Ufaransa yenye umoja." Katika matamshi yake hayo Rais wa Ufaransa aliendelea kudai kuwa anakusudia kuzuia ushawishi wa pande za kigeni kwa Waislamu wa nchi hiyo.

Kiujumla muswada huo una lengo la kuimarisha mielekeo ya kisekulari na kutenganisha baina ya taasisi za kidini yakiwemo makanisa, na serikali. Vilevile unajumuisha suala la kukabiliana na uwekezaji wa kigeni katika ujenzi wa misikiti na shule za kidini na kupambana na maimamu wa misikiti ambao wana uraia wa kigeni nchini Ufaransa.
Akijibu madai kwamba lengo la muswada huo ni kukabiliana na vitendo vya kuzusha migawanyiko, Kamel Kabtane msimamizi wa msikiti wa Lyon huko Ufaransa amehoji: "Ni kitu gani kinasabababisha migawanyiko? Waislamu si chanzo cha migawanyiko katika jamii bali wanataka umoja na mshikamano.
Madai yasiyo na msingi yaliyotolewa na Macron kuhusu kuwepo eti hali ya mgogoro katika dini ya Kiislamu ulimwenguni yametolewa katika hali ambayo, kinyume na matamshi hayo yasiyo na mashiko wala msingi wowote, takwimu zinaonyesha kwamba dini ya Uislamu inakuwa na kustawi kwa kasi kubwa barani Ulaya na idadi ya Waislamu imeongezeka sana. Hali hii pia inashuhudiwa waziwazi katika uga wa kimataifa. Wakati huo huo Macron amedai kupambana na kile alichokitaja kuwa ni "misimamo mikali ya Kiislamu" ilhali tunapotupia jicho matukio ya muongo mmoja wa karibuni tunaona kuwa, baadhi ya nchi za Ulaya kama Ufaransa, Uingereza na Marekani zilikuwa na mchango mkubwa sana katika kuanzisha makundi ya kigaidi na kitakfiri kama lile la Daesh. Lengo la Wamagharibi lilikuwa kuwatumia magaidi hao kama wenzo ili kufanikisha malengo yao katika eneo magharibi mwa Asia hususan kukabiliana na mhimili wa muqawama katika eneo hilo kupitia njia ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Syria. Hata hivyo wameshindwa kutimiza lengo hilo, na katika miaka kadhaa ya karibuni magaidi hao wa Daesh waliwageuka mabwana zao kwa kuhamishia mashambulizi yao katika nchi za Ulaya zilizokuwa zikiwaunga mkono na kuwafadhili. Sasa moto uliowashwa na nchi za Ulaya umezizingira nchi hizo zenyewe.

Suala jingine ni kwamba, Macron amewasilisha mpango wake huo mpya akidai kuwa utaimarisha mtengano baina ya siasa na dini na kuzidhoofisha taasisi za Kiislamu kama misikiti. Hata hivyo, kwa mpango huo pia serikali ya Ufaransa imefungua milango ya hujuma na mashambulizi dhidi ya Uislamu na Waislamu. Mfano wa wazi wa jambo hilo ni hatua ya karibuni ya jarida la Charlie Hebdo la Ufaransa la kuchapisha tena vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume mtukufu wa Uislamu, Muhammad (s.a.w). Baada ya malalamiko makali na ukosoaji mkubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu dhidi ya kitendo cha jarida hilo, Rais Emmanuel Macron alitoa matamshi ya kifedhuli akisema kuwa hatua ya jarida hilo ni "uhuru wa kusema" na kudai kuwa anatetea uhuru huo. Haijulikani Rais wa Ufaransa alikuwa akimaanisha nini kuhusu neno "uhuru wa kusema?" Je uhuru wa kusema una maana ya udhalilishaji, matusi na kudhihaki matukufu ya zaidi ya Waislamu bilioni moja na nusu ulimwenguni kote? Na je matusi na kuvunjia heshima matukufu ya Waislamu ndivyo vinavyoonesha kuwepo uhuru wa kusema nchini Ufaransa? Kama ni hivyo basi kwa nini waandishi na watafiti kama Profesa Roger Garaudy wamehukumiwa vifungo jela kwa sababu tu ya kutilia shaka kadhia ya Holocaust?

Ukweli wa mambo ni kuwa uhuru katika mtazamo wa wanasiasa kama Emmanuel Macron una maana ya upande mmoja yaani uhuru wa kupinga na kuhujumu Uislamu.