Dec 31, 2022 13:20 UTC
  • Kumbukumbu ya Siku ya Kuanzishwa Harakati ya Kupambana na Ujinga nchini Iran

Moja kati ya haki za msingi za binadamu katika jamii yoyote ile ni kujua kusoma na kuandika.

Kila mtu, ikiwa ni pamoja na watoto, vijana na watu wazima, wanapaswa kuwa na fursa za kupata elimu na maarifa. Hitajio hilo linajumuisha kuwa na uwezo wa kusoma na kuandika, na ndio sababu ya ustawi na maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni katika kila jamii. Uwezo wa kusoma na kuandika humuunganisha mwanadamu na nyakati zilizopita, za sasa na zijazo na humpa uwezo wa kurekodi, kusajili na kuhamisha au kutoa uzoefu na ujuzi na maarifa yake katika jamii.

Inasikitisha kuona kuwa, kulingana na takwimu zilizochapishwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika bado kiko juu katika baadhi ya nchi zinazoendelea. Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa mwaka 1976, nchini Iran, kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, zaidi ya asilimia 50 ya watu walikuwa hawajui kusoma na kuandika. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kulichukuliwa hatua makhsusi za kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika, hasa watu wazima na watoto wasio na uwezo wa kwenda shule. Miongoni mwa hatua hizo ni kuanzishwa kwa Jumuiya ya Harakati ya Kusoma na Kuandika ya Iran (Literacy Movement Organization of Iran) kwa amri ya mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Ayatullah Imam Ruhullah Khomeini (RA), tarehe 27 Disemba 1979. 

Neno na amri ya kwanza ya Mwenyezi Mungu katika "Qur'ani tukufu, kitabu cha mwisho cha Mwenyezi Mungu, ni amri ya kusoma. Amri na wajibu huu pia umesisitizwa sana na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) kwa Waislamu wote. Alilipa umuhimu mkubwa suala la kupiga vita ujinga na udharura wa kujua kusoma na kuandika kiasi kwamba alilifanya suala hilo kuwa kikomboleo cha washirikina waliotekwa nyara katika vita vya Badr. Mtume (saw) alimwaamuru kila mateka wa washirikina wa Makka aliyekuwa akijua kusoma na kuandika kuwafundisha kusoma na kuandika Waislamu 10 kama gharama ya kukombolewa na kuachiwa huru. Ni kwa mtazamo huo ndiyo maana kutafuta elimu ni wajibu katika dini ya Uislamu. Hivyo Muislamu asiyefuata lengo hili la kutafuta elimu na maarifa huwa amekiuka amri na faradhi ya dini, na kinyume chake, watafutaji elimu wamepewa bishara za malipo mema. 

Kutokana na mtazamo huo wa Kiislamu, katika miezi ya mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ruhullah Mussawi Khomeini (RA) alitoa amri ya kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika. Sehemu moja ya amri na dikrii ya Imam Khomeini kwa mnasaba huu inasema: "Ni jambo la aibu katika nchi hii ambayo ilikuwa chimbuko la elimu na fasihi na inayoishi katika kivuli cha Uislamu unaotambua suala la kutafuta elimu kuwa ni faradhi na wajibu, kuwapo watu wasiojua kusoma na kuandika. Tunapaswa kubadilisha utamaduni tegemezi wa nchi yetu kuwa utamaduni unaojitegemea na unaojitosheleza kupitia mpango wa muda mrefu. Sasa, bila kupoteza wakati, tunapaswa kusimama mara moja kupambana na suala la kutojua kusoma na kuandika .. ili, kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu, katika siku za usoni, kila mtu awe na elimu ya awali ya kuandika na kusoma."  

Katika dikrii hiyo ya Imam Khomeini kunaonekana malengo mawili yenye thamani. Kwanza, ni kuwafundisha kusoma na kuandika watu walionyimwa neema yenye thamani kubwa ya kusoma na kuandika, na pili, kuboresha na kunyanyua juu ujuzi na maarifa ya watu wazima wanaojua kusoma na kuandika katika nyanja mbalimbali na kubadilisha utamaduni tegemezi wa nchi kuwa utamaduni unaojitegemea na unaojitosheleza.   

Kufuatia amri hiyo, iliundwa Jumuiya ya Harakati ya Kusoma na Kuandika na kuanza kutekeleza mipango mbalimbali, na imeweza kutimiza amri ya kihistoria ya Imam Khomeini katika miaka 40 iliyopita. Kiwango cha watu waliokuwa wakijua kusoma na kuandika nchini Iran baina ya wananchi waliokuwa na umri wa miaka 6 na kuendelea hapo mwaka 1976 ambacho kilikuwa asilimia 47.5 kiliongezeka na kufikia asilimia 79.5 katika sensa ya mwaka 1996 na mwenendo huo uliendelea katika miaka iliyofuata. Sensa ya mwaka 2016 hapa nchini ilionesha kuwa mwaka 2016 asilimia 87.6 ya Wairani walikuwa na uwezo wa kusoma na kuandika na takwimu za mwaka 2019 zilibaini kuwa kiwango hicho kimeongezeka na kufikia asilimia 89. Tangu wakati huo kulichukuliwa hatua nyingine ya kutimiza malengo ya harakati hiyo ya kimapinduzi yaani elimu, ujuzi na maarifa ya baada ya kujua kusoma na kuandika. 

Hii leo, vigezo vya ustawi na maendeleo ya nchi yoyote vinaonesha kuwa ili kuweza kupata maendeleo endelevu, kuna ulazima wa kwenda mbali zaidi ya kupata ujuzi wa kusoma na kuandika. Hii ina maana kwamba, idadi na asilimia ya juu ya watu wanaojua kusoma na kuandika peke yake havitoshi; bali jambo lenye umuhimu zaidi ni kwa wale waliopata ujuzi huo wa awali wa kusoma na kuandika kufungua dirisha la maarifa, sayansi na teknolojia na kufanya mabadiliko katika jamii zao. Ni kuona wakibadilisha hali zao wao wenyewe, familia, jamii na nchi na kupiga hatua za kuboresha hali ya jamii katika masuala ya ajira, uchumi, siasa na utamaduni; vinginevyo, ndoto ya kufikia kwenye vilele vya maendeleo na ustawi itabaki kama kaulimbiu tupu. 

Kutokana na umuhimu wa suala hili, Jumuiya ya Harakati ya Kusoma na Kuandika ya Iran ilianza kufundisha ujuzi na stadi mpya kulingana na malengo yake. Suala hili pia limepewa umuhimu maalumu na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), ambalo tangu mwaka 1967 limekuwa likiwaenzi na kuwakirimu watu au jumuiya zilizofanya vizuri katika medani hiyo. Inatupasa kukumbusha hapa kuwa, katika kipindi cha miongo minne iliyopita Harakati ya Kusoma na Kuandika ya Iran (Literacy Movement Organization of Iran) imepewa tuzo nyingi za UNESCO. Miongoni mwa tuzo hizo ni Tuzo ya UNESCO ya "Noma" (The Noma Literacy Prize) kwa utekelezaji wa Mradi wa Uhamasishaji wa Kusoma na pia utekelezaji wa Mpango wa Mafunzo ya Stadi za Maisha kwa wasichana wanaofanya kazi vijijini, Tuzo ya UNESCO ya "King Sejong" (King Sejong Literacy Prize) kwa utekelezaji wa mradi wa kuimarisha stadi za kusoma na kuandika, kuhimiza kujisomea na kukuza stadi za kazi na mahusiano ya kifamilia, na tuzo ya kimataifa ya UNESCO ya " Malcolm Adiseshiah" (Malcolm Adiseshiah International Literacy Prize) kwa kufanikisha usanifu na utekelezaji wa mradi wa huduma ya mawasiliano ya kusoma na kuandika.

Katika suala hili, moja ya stadi zinazotekelezwa na Jumuiya ya Harakati ya Kusoma na Kuandika ya Iran katika miaka ya hivi karibuni, ni kujumuisha pamoja ujuzi wa kusoma na kuandika na stadi za kompyuta. Hii leo, dhana mpya ya kujua kusoma na kuandika inajumuisha ujuzi na stadi za kompyuta, maarifa ya teknolojia, habari na mawasiliano na kadhalika. Kazi na mafanikio ya Iran katika uwanja huu ni makubwa sana kwa kadiri kwamba imepongezwa na shirika la UNESCO. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Sekretarieti ya Tuzo za Kimataifa za UNESCO, mradi wa kuchanganya kusoma na kuandika na stadi za kimsingi za kompyuta katika kipindi cha mpito" uliowasilishwa na Shirika Harakati ya Kusoma na Kuandika ya Iran hapo mwaka 2018, ulifanikiwa kupata tuzo ya kimataifa ya Confucius (Confucius Prizes for Literacy) pamoja na miradi mingine kutoka Nigeria, Uhispania, Afghanistan, na Uruguay. Bodi iliyotathmini programu hiyo ilisema kuwa, sababu kuu ya kuchaguliwa mradi huo wa Iran ni kujikita kwake katika kufundisha misingi ya taaluma ya kompyuta kwa wanawake na kuboresha uwezo wa kusoma na kuandika wa tabaka hilo muhimu la jamii na kuwawezesha katika uwanja wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Hapana shaka yoyote kwamba, shughuli za Jumuiya ya Harakati ya Kusoma na Kuandika ya Iran nchini Iran zitaendelea bila kusita hadi hali ya kutojua kusoma na kuandika itakapotokomezwa kikakmilifu nchini Iran, sambamba na kazi za Wizara ya Elimu. 

Tags