Museveni aituhumu UN kuwa 'inalinda ugaidi' Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39101-museveni_aituhumu_un_kuwa_'inalinda_ugaidi'_kongo_dr
Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameibua tuhuma nzito dhidi ya Umoja wa Mataifa akidai kuwa chombo hicho cha kimataifa 'kinalinda ugaidi' mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 17, 2018 11:14 UTC
  • Museveni aituhumu UN kuwa 'inalinda ugaidi' Kongo DR

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameibua tuhuma nzito dhidi ya Umoja wa Mataifa akidai kuwa chombo hicho cha kimataifa 'kinalinda ugaidi' mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Museveni alitoa tuhuma hizo jana baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa UN wanaochunguza mauaji ya askari 20 wa kikosi cha kulinda amani cha umoja huo nchini Kongo mwezi uliopita.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais wa Uganda hata hivyo haijafafanua ni jinsi gani Umoja wa Mataifa unalinda harakati za ugaidi mashariki mwa Kongo DR.

Itakumbukwa kuwa,  askari 15 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  na watano wa DRC waliuawa mwanzoni mwa mwezi uliopita wa Disemba, katika kambi ya Semuliki mkoani Kivu Kaskazini kufuatia hujuma ya waasi hao wa ADF.

Waasi wa ADF Nalu wanaoendesha harakati zao mashariki mwa DRC

Uganda na Kongo DR zilikubaliana kushirikiana kupambana na waasi wa ADF wanaotokea Uganda ambao wanaendesha harakati zao mashariki mwa DRC baada ya hujuma hiyo, na hivi karibuni zilizindua operesheni ya pamoja.

Wanajeshi wa Tanzania na Kongo waliouawa katika mashambulizi hayo ya mapema mwezi jana walikuwa sehemu ya askari 3,000 wa timu ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa MONUSCO yenye askari kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.