Amir-Abdollahian: Uwepo wa dola la Kizayuni umeitia kwenye matatizo makubwa dunia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i105520-amir_abdollahian_uwepo_wa_dola_la_kizayuni_umeitia_kwenye_matatizo_makubwa_dunia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Ghaza zimeiweka kwenye alama ya kuuliza itibari ya jamii ya kimataifa na madai ya kupigania haki za binadamu ulimwenguni.
(last modified 2023-12-02T07:15:02+00:00 )
Dec 02, 2023 07:15 UTC
  • Amir-Abdollahian: Uwepo wa dola la Kizayuni umeitia kwenye matatizo makubwa dunia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Ghaza zimeiweka kwenye alama ya kuuliza itibari ya jamii ya kimataifa na madai ya kupigania haki za binadamu ulimwenguni.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo na kuongeza kuwa, janga la Palestina lililoanzia mwaka 1948 kwa kutangazwa dola pandikizi la Kizayuni katika ardhi za Wapalestina, linaendelea hadi hivi sasa na jinai nyingi zilizofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina zimepotea kwenye historia na nyingine nyingi zimefifilizwa na kusahaulishwa kwa makusudi na wanasiasa. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, matukio ya Oktoba 7, 2023 hayakuzuka vivi hivi bila ya sababu maalumu na ni jambo lisilo na shaka hata kidogo kwamba haki za taifa madhlumu za Palestina zinakanyagwa kwa muda mrefu hasa baada ya mwaka 1948 wakati lililpoundwa dola la Kizayuni. Amesema, kwa kuzingatia yote hayo tutaona kuwa, taifa la Palestina lina haki zote za kuendesha mapambano  ya kukomboa ardhi zake.

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

 

Ameongeza kuwa, kinachotokea Ukanda wa Ghaza hivi sasa kwa hakika ni muendelezo wa jiinai za makumi ya miaka za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Hivyo operesheni ya #Kimbunga_cha_al Aqsa iliyoendeshwa kishujaa na wanamapambano wa Palestina tarehe 7 Oktoba 2023, ni mapambano ya haki ya kukabiliana na jinai za kuchupa mipaka za makumi ya miaka za utawala wa Kizayuni.

Vile vile amesisitiza kuwa, leo hii jamii ya kimataifa inashuhudia kwa macho yake jinsi njia zote za kimataifa zilivyoshindwa kuyatendea haki mataifa yanayodhulumiwa duniani na jinsi sheria hizo zilivyoshindwa kuleta amani na usalama ulimwenguni.

Jumamosi ya tarehe 7 Oktoba 2023, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS iliendesha operesheni ya kishujaa ya #Kimbunga_cha_al Aqsa na kutoa pigo kubwa la kiusalama, kijeshi na kiuchumi kwa utawala pandikizi na mtenda jinai wa Israel.

Utawala dhalimu wa Israel ambao umeshindwa kwenye medani za mapambano, umeamua kumalizia hamaki zake kwa kuua watoto wachanga, watoto wadogo, wanawake, vizee na raia wa kawaida huko Ghaza.