Kan'ani: Marekani ndiyo inayopaswa kubeba dhima ya jinai za Israel huko Palestina, Lebanon na Syria
(last modified Sun, 22 Sep 2024 02:59:09 GMT )
Sep 22, 2024 02:59 UTC
  • Kan'ani: Marekani ndiyo inayopaswa kubeba dhima ya jinai za Israel huko Palestina, Lebanon na Syria

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya ya Iran amesema kuwa, Marekani ndiyo inayopaswa kubeba dhima na kujibu malalamiko makubwa ya kimataifa kwa kushiriki kwake katika jinai za utawala wa Kizayuni huko Palestina, Lebanon na Syria.

Nasser Kan'ani amegusia pia mauaji ya umati yanayofanywa na utawala wa Kizayuni ikiwa ni pamoja na ya siku za hivi karibuni huko Lebanon, Syria na Palestina na kuandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba, pamoja na utawala wa Kizayuni kufanya jinai na unyama wa kutisha ambao haujawahi kushuhudiwa mfano wake, lakini Marekani inaendelea kuiunga mkono kibubusa Israel, kisiasa, kijasusi, kiusalama na katika kila kitu ikiwa ni pamoja na kuzuia maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala unaotenda jinai kubwa wa Kizayuni. 

Hii ni kusema kuwa, Ijumaa usiku, Marekani kwa mara nyingine tena iliunga mkono kwa uwazi kabisa jinai za Israel katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo liliitisha kikao cha kujadili mashambulizi ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni huko Lebanon yaliyoua kwa umati raia wasio na hatia.

Juzi Ijumaa, utawala wa Kizayuni ulifanya shambulio jengine la kigaidi kusini mwa Lebanon kwa kushambulia jengo moja la makazi ya raia na kuua shahidi wananchi 31 wa Lebanon na kujeruhi wengine 76. 

Siku za Jumanne na Jumatano (Septemba 17 na 18) utawala katili wa Kizayuni uliripua idadi kubwa ya vifaa vya kupokea ujumbe (pagers) nchini Lebanon hususan katika mji mkuu Beirut. Watu 37 ikiwa ni pamoja na msichana mdogo waliuawa shahidi na wengine wapatao elfu nne walijeruhiwa, wakiwemo waliopoteza viungo mbalimbali vya mwili.

Tags