Burkina Faso: Hatua ya Trump dhidi ya Quds inapaswa kuzuiwa
Naibu Spika wa Bunge la Burkina Faso ametoa mwito wa kusimamishwa utekelezwaji wa mpango wa Marekani wa kuuhamishia mjini Quds Tukufu, ubalozi wake ulioko Tel Aviv.
Salifu Timore aliyasema hayo jana Jumamosi katika mazungumzo na Spika wa Bunge la Iran, Ali Larijani, pambizoni mwa mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Mabunge ya Nchi za Kiislamu wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu PUIC unaofanyika hapa mjini Tehran.
Ameitaja hatua hiyo ya Marekani dhidi ya Quds kuwa kitendo cha hatari, ambacho kinapaswa kuzuiwa kwa nguvu zote, huku akitoa mwito wa umoja na mshikamano miongoni mwa nchi za Kiislamu dhidi ya sera za uhasama na za kichokozi za Washington.
Itakumbukwa kuwa tarehe 6 Disemba mwaka jana, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza Quds Tukufu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na kueleza kuwa atauhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Quds.
Chokochoko hiyo ya Trump iliibua ghadhabu na malalamiko sio tu katika ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu, bali kote duniani.
Kwa upande wake, Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu mbali na kueleza utayarifu wa Iran kuimarisha uhusiano wa pande mbili na Burkina Faso, ameitaja hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitambua Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa Israel kama kitendo cha ubaguzi.
Wakati huo huo, Naibu Spika wa Bunge la Burkina Faso amesema mpango wa kuufungua upya ubalozi wa nchi yake hapa Tehran upo katika hatua za juu, na karibuni hivi ujumbe wa kutathmini suala hilo utaitembelea Iran.