Mar 27, 2024 07:38 UTC
  • Israel yapuuza azimio la Baraza la Usalama, yadondosha mabomu Rafah

Jeshi katili la Israel limeendelea kuushambulia kwa mabomu mji wa Rafah wa kusini mwa Ukanda wa Gaza, licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupasisha azimio la kusimamisha vita huko Gaza baada ya miezi sita ya mashambulizi ya jeshi la utawala huo wa Kizayuni katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa kanali ya al-Jazeera, vifaru na magari ya deraya ya utawala wa Kizayuni yameizingira hospitali moja mjini Khan Younis, huku Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina likiripoti kuwa, kituo kingine cha afya kimesitisha shughuli zake kutokana na operesheni hizo ya wanajeshi makatili wa Israel katika eneo hilo.

Shirika la habari la Wafa limeripoti habari ya kuuawa shahidi Wapalestina watatu katika vijiji vya Khirbet al-Adas na ash-Sha’out viungani mwa Rafah, mbali na kijana mwingine wa Kipalestina kuuawa kwa kupigwa risasi katika mji wa Jenin.

Kadhalika askari za Kizayuni wamewapiga risasi vijana wanne wa Kipalestina katika mji wa Qabatiya, kusini mwa Jenin. Halikadhalika utawala huo pandikizi umeshambulia kwa mabomu maeneo ya kusini mwa Lebanon na kuua watu saba. 

Hujuma za kikatili za Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza

Utawala pandikizi wa Israel mbali na kufumbia macho azimio la juzi Jumatatu la Baraza la Usalama, lakini pia umepuuza utekelezaji wa azimio nambari 2720 lililopasishwa na baraza hilo Disemba 2023, la kutaka kufikishwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Kabla ya hapo pia, utawala haramu wa Israel ulidharau uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wa kuutaka uchukue hatua zote zinazohitajika kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, na badala yake jeshi la utawala huo pandikizi limeendelea kumwaga damu za Wapalestina wa Gaza.

Tags