Upinzani wa Wamagharibi kwa usitishaji vita Gaza
(last modified Tue, 14 Nov 2023 09:23:43 GMT )
Nov 14, 2023 09:23 UTC
  • Upinzani wa Wamagharibi kwa usitishaji vita Gaza

Licha ya kupita karibu siku 40 tangu ilipotokea operesheni ya kimbunga ya Al-Aqswa na radiamali ya utawala wa Kizayuni kwa operesheni hiyo kwa kushambulia kwa mabomu Ukanda wa Gaza na kuuawa maelfu ya Wapalestina na uharibifu mkubwa wa eneo hilo, lakini baadhi ya madola ya Magharibi yakifungamana na Waziri Mkuu wa utawala huu, Benjamin Netanyahu, bado yangali yanapinga usitishaji wa vita hivi vya umwagaji damu.

Olaf Scholz Kansela wa Ujerumani ni mmoja wa wapinzani wakubwa wa kusitishwa kwa mapigano mara moja katika Ukanda wa Gaza. Kansela wa Ujerumani alisema siku ya Jumapili kwamba, haoni kama mwito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja katika Ukanda wa Gaza ni sahihi, kwani kufanya hivyo kutaipa Harakati ya Hamas fursa ya kukusanya nguvu.

Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani ameunga mkono kusitishwa vita kwa muda mfupi kwa ajili ya masuala ya kibinadamu na kuruhusu kusafirishwa majeruhi na kupeleka misaada kwa wakaazi wa Ukanda wa Gaza.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sonak, sambamba na kupinga kusitishwa kwa mapigano katika vita vya Gaza, alimfuta kazi afisa wa serikali kwa kutoa mwito wa kuweko usitishaji vita wa "kudumu" huko Gaza. London imekataa kutoa wito wa kukomesha vita huko Gaza, na imetoa pendekezo la usitishaji vita wa muda mfupi tu ili kuruhusu misaada kufika eneo linalozingirwa na Gaza.

Marekani ikiwa ni muungaji mkono muhimu zaidi wa utawala wa Kizayuni, imepinga vikali usitishaji vita wa Gaza, na kwa kuzingatia kile kinachodaiwa haki ya Israel ya kujilinda, imetoa idhini kwa Tel Aviv kuendesha vitendo vya kigaidi kama vile kulenga hospitali, na mahali pa kukutanikia watu waliokimbia makazi yao wa Gaza ambao wamekimbilia katika maeneo na vituo vya Umoja wa Mataifa.

 

Pamoja na hayo, Rais Joe Biden wa Marekani hivi karibuni alitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kwa siku tatu huko Gaza ili kuachiliwa huru mateka wito ambao ulikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Netanyahu. Hata hivyo, Ijumaa, Novemba 10, Biden alidai kuwa, utawala wa Kizayuni utakubali "kusitishwa vita kwa malengo ya kibinadamu" baada ya kushinikizwa na Washington.

Madai haya yanatolewa huku Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni akisisitiza kuwa: "bila ya kuachiliwa huru mateka wa Israel, hakutakuweko na suala la usitishaji vita huko Gaza."

Hii ni katika hali ambayo, mwanzoni mwa Vita Biden alisafiri kwenda Palestina inayokaliwa kwa mabavu chini ya urushaji wa roketi na makombora ya HAMAS ambapo alitangaza kumuunga mkono Netanyahu na kutangaza dhamira ya Washington ya kuilinda Israel. Lakinii pamoja na hayo, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni hakuwa tayari kukubali hata ambalo kimsingi sio muhimu sana la Biden la kusitishwa vita kwa muda kwa sababu za kibinadamu. Nukta ya kuzingatia ni hii kwamba, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ambaye hivi karibuni alitaka kusimamisha mashambulio dhidi ya Gaza, amebadilisha msimamo wake kufuatia radiamali ya utawala wa Kizayuni.

 

Macron alisema katika mahojiano aliyofanyiwa ya kwamba, Israel inapaswa kuacha kuua watoto na wanawake huko Gaza kwa sababu "hakuna uhalali" kwa namna yoyote wa mashambulizi haya ya mabomu na kwamba, usitishaji vita huo utakuwa kwa maslahi ya Israel. Lakini siku ya Jumapili, Macron alibadilisha mia kwa mia msimamo wake katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Rais wa utawala wa Kizayuni, Isaac Herzog, ambapo katika msimamo wake wa awali alikuwa amewakosoa vikali Wazayuni.  Macron alikuja na madai mapya kwa kusema kwamba, haitambui Israel kama mhusika wa mateso na masaibu ya Wapalestina katika mashambulio ya jeshi la Israel huko Gaza.

Hili linaonyesha kuwa, lobi za Wazayuni zina taathira katika uga wa kisiasa wa nchi za Ulaya ikiwemo Ufaransa na wakuu wa nchi hizo kwa kutaka au kutotaka hulazimika kufuata misimamo ya utawala wa Kizayuni katika maamuzi yao.