UN yazitaka India na Pakistan ziruhusu uchunguzi Kashmir
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza masikitiko ya umoja huo baada ya serikali za Pakistana na India kukataa kuwapa kibali maofisa wa UN kulitembelea eneo lenye mzozo la Kashmir, katika mpaka wa nchi mbili hizo.
Zeid Ra’ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema juhudi za UN za kutaka waangalizi wake walitembelee eneo la Kashmir ili kufanya uchunguzi kuhusu madai ya mauaji na ukandamizaji unaofanywa na maafisa usalama, zimegongwa mwamba.
Kamishna huyo wa UN amesema umoja huo unataka kutuma maofisa wake wakafanye uchunguzi huru juu ya madai hayo ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo hilo.
Watu wasiopungua 60 wameuawa hadi sasa katika machafuko yaliyoanza Julai 9 katika eneo hilo huku wengine 3,500 wakijeruhiwa. Wanajeshi na maofisa wa polisi wa India wanadaiwa kutumia nguvu kupita kiasi kuwakandamiza waandamanaji ambao wamekuwa wakitoa nara za kutaka uhuru. Maandamano hayo yalianza baada ya Wani, kiongozi mwandamizi wa chama cha kupigania uhuru wa Kashmir, Hizb ul Mujahideen, kuuawa akiwa na watu wengine wawili baada ya kufyatuliana risasi na wanajeshi wa India katika eneo hilo.
Kashmir ni jimbo lenye Waislamu wengi India na limekuwa likikumbwa na mzozo tokea India ipate uhuru kutoka Uingereza mwaka 1947. Eneo lingine la Kashmir liko Pakistan ambayo pia ilikuwa koloni la Uingereza.