Saudia yaichochea Israel iihujumu Lebanon, Hizbullah yasema iko tayari kijeshi
Afisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, harakati hiyo iko tayari kwa ajili ya makabiliano yoyote ya kijeshi huku kukiwa na tetesi kuwa Saudi Arabia inauchochea utawala wa Kizayuni wa Israel uishambulie Lebanon kijeshi.
Akizungumza Jumatatu, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la Hizbullah Sheikh Nabil Qauoq amesema: "Adui Muisraeli anafahamu vyema matokeo mabaya ya hujuma yoyote dhidi ya Lebanon na hawezi kustahamili hali hiyo."
Ameongeza kuwa, Haraakti ya Hizbullah imesimama imara huku ikiwa tayari kwa chochote kinachoweza kutokea. Hizbullah ina uwezo kamili wa kupata ushindi na kumrudisha nyuma mvamizi."
Akizungumza siku ya Ijumaa, Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyed Hassan Nasrullah alifichua kuwa, Saudi Arabia imeiomba Israel ianzishe mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Lebanon kwa kisingizio cha kukabiliana na Hizbullah na kwamba watu wa Saudia wako tayari kutumia mabilioni ya dola kufikia lengo hilo.
Sayyed Nasrullah amesema, Saudia inaogopa kukabiliana ana kwa ana kijeshi na Iran hivyo inataka kulipiza kushindwa kwake huo kupitia kuishambulia Hizbullah.