Abbas: Quds inaweza kuwa lango la amani au vita, Trump achague
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas amesema mji wa Baitul Muqaddad unaweza kuwa lango la kupatikana amani au kuibua vita, na Marekani ina khiari ya kuchagua njia inayoitaka.
Abbas aliyasema hayo jana Jumatano katika Kongamano la Kimataifa la Quds la al-Azhar mjini Cairo ambapo ameitaja kama 'dhambi' hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuitangaza Quds Tukufu kuwa mji wa mkuu Israel.
Amesisitiza kuwa serikali ya Marekani imepoteza nafasi yake ya kuwa mpatanishi katika mchakato wa kutatua mgogoro kati ya Palestina na Israel na kukariri kwamba Washington imekiuka sheria na maazimio ya kimataifa kutokana na hatua yake hiyo ya kichokozi.
Jamii ya kimataifa zikiwemo nchi nyingi waitifaki wa Marekani imelaani hatua iliyochukuliwa tarehe 6 mwezi uliopita wa Disemba na Rais Donald Trump wa Marekani ambaye, kinyume na maazimio ya kimataifa, aliitangaza Quds Tukufu (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.
Aidha alitangaza kuwa Marekani imeanzisha mchakato wa kuuhamishia ubalozi wake katika mji huo kutoka Tel Aviv.