Oct 27, 2023 07:27 UTC
  • Kupigiwa kura ya veto maazimio yanayohusu vita vya Ghaza katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena limeshindwa kupasisha azimio Katika hali ambayo wananchi wa Ukanda wa Ghaza bado wanakabiliwa na mashambulizi ya kinyama na ya kutisha ya utawala wa Kizayuni ambapo utawala huo unazuia kufikishwa misaada ya dharura katika eneo hilo.

Azimio lililopendekezwa na Russia katika Baraza la Usalama kwa ajili ya kusimamishwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza hayakupasishwa Jumatano jioni kutokana na kupingwa na nchi za Magharibi. Azimio hilo lililopendekezwa lilipigiwa kura ya turufu na Marekani kutokana na siasa za uungaji mkono wa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani kwa jinai za utawala huo dhidi ya Wapelastina.

Vasily Nebenzya mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa alisema katika kikao hicho kuwa: "Tunasikitika kwamba baraza hili limeshindwa kutumia fursa nyingine kushughulikia mzozo wa Mashariki ya Kati."

Huku akibainisha kuwa maslahi finyu ya nchi za Magharibi katika kuiunga mkono Tel Aviv yanazuia kusimamishwa kwa mashambulizi ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Ghaza, Nebenzia ameezea kuwa Marekani haitaki maazimio ya Baraza la Usalama yaiathiri Israel.

Hii ni pamoja na kuwa kabla ya hapo jitihada za Marekani za kupasisha azimio lake kuhusisana na mgogoro wa Ghaza ambalo lilitoa uungaji mkono wa wazi kwa utawala wa Kizayuni na lilikuwa dhidi ya Wapalestina lilikabiliwa na kura ya veto ya Russia na China. Azimio hilo lilipendekeza suala la kutumwa misaada ya kibinadamu huko Ghaza, lakini halikuashiria kusimamishwa mashambulizi na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ghaza. Azimio la Marekani pia lilitaka kulaaniwa Hamas kutokana na operesheni yake ya Kimbunga cha Al-Aqsa na kusisitiza juu ya eti haki ya Israel kujilinda.

 Vasily Nebenzya Mwakilishi wa Russia katika Baraza la Usalama 

Mwakilishi wa Russia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema: Azimio lililopendekezwa na Marekani ni kama kutolewa ruhusa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuendelea mashambulizi ya Israel dhidi ya Ghaza. Mwakilishi  wa China naye pia alisisitiza kuwa azimio lililopendekezwa na Marekani linahalalisha kutumiwa  nguvu na silaha dhidi ya raia wasiokuwa na hatia wa Palestina.

Ameongeza kuwa Azimio lolote lenye utata kuhusu vita na amani ni la kutowajibika, ni hatari na linafungua njia kwa operesheni kubwa za kijeshi.

Misimamo ya Russia na China dhidi ya siasa za nchi za Magharibi zinazoongozwa na Marekani za kuunga mkono vitendo vya jinai za utawala wa Kizayuni, imepongezwa na Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya kisiasa ya Hamas na vilevile nchi wanachama na zisizo wanachama wa Baraza la Usalama, zinazotaka kusitishwa mara moja mashambulizi makali ya kinyama dhidi ya raia wa Ghaza.

Haniyeh ameitaka Jamii ya Kimataifa kuushinikiza utawala wa Kizayuni kuheshimu haki za binadamu na kutekeleza sheria na maazimio ya kimataifa na ya kibinadamu kwa ajili ya haki za wananchi wa Palestina hususan watu wa Ghaza.

Inaonekana kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa katika kazi yake kuu ya kudumisha amani na usalama wa kimataifa na kukomesha migogoro ya kieneo. Kwa kuzingatia  kura ya turufu ya wanachama 5 wa kudumu wa baraza hilo, yaani Marekani, Uingereza, Ufaransa, Russia na China, inaonekana kuwa itakuwa vigumu sana kufikia maoni ya pamoja juu ya vita vya Ghaza, ambayo yatazikurubisha  nchi hizo na zinginezo ambazo si wanachama wa Baraza la Usalama.

Hali ya kusikitisha ya wakazi wa Ghaza

Wakati huo huo, nafasi ya nchi za Magharibi wanachama wa Baraza la Usalama zikiongozwa na Marekani iko wazi katika kutozuia kuendelea kuuawa watu wa Ghaza na utawala wa Kizayuni. Marekani, ikiwa kama muungaji mkono muhimu wa Israel, imeipa bila masharti Tel Aviv ruhusa ya kuendeleza mauaji na uharibifu huko Ghaza kwa kupinga maazimio ambayo yanataka kusitisha mapigano katika eneo hilo.

Vasily Nebenzia, ​​Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, alisema katika kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya Asia Magharibi kwamba matukio ya kusikitisha ya eneo hili yanatokana na siasa za muda mrefu za uharibifu za Washington na sera zake za kuvuruga michakato ya amani na usalama ya kutatua masuala ya vita vya muda mrefu katika eneo hilo.

Katika kukabiliana na kushindwa kijeshi, kiusalama na kijasusi na Hamas pamoja na makundi mengine ya muqawama ya Palestina katika operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, utawala wa Kizayuni umeshambulia kinyama kwa mabomu maeneo ya makazi na vituo vya umma eneo la Ukanda wa Ghaza, na matokeo yake ni kuuawa shahidi zaidi ya Wapalestina elfu sita  na zaidi ya wengine elfu 20 pia wamejeruhiwa. Kuendelea hali hiyo na kushindwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua katika uwanja huo kunaweza kusababisha maafa makubwa zaidi ya kibinadamu katika karne ya 21.

 

Tags