Austria yaikosoa vikali Marekani kutokana na kujiondoa katika JCPOA
Kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA Mei mwaka huu, hatua ambayo ilichukuliwa na Rais Donald Trump wa nchi hiyo, kulifuatiwa na ukosoaji mkubwa wa nchi zingine wanachama wa kundi la 5+1 zikiwemo nchi tatu za Troika ya Ulaya za Ufaransa, Uingereza na Ujerumani.
Hata hivyo sio nchi tatu hizo pekee za Ulaya zilizolalamikia hatua hiyo iliyokinzana na vigezo vya kimataifa, bali nchi nyingine pia wanachama wa Umoja wa Ulaya ambazo zina uhusiano mpana na Iran zilikosoa vikali hatua hiyo ya Trump. Kuhusiana na hilo, Karin Kneissl, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Austria amesema kuwa, kwa mtazamo wa kisheria, kujitoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa na ni "uangamizaji wa makubaliano yaliyokuwa na mafanikio".
Bi Karin Kneissl ameandika makala akitetea makubaliano ya JCPOA ambapo sehemuu moja ya makala hiyo inasema: Hata akichukua hatua ya upande mmoja (akimkusudia Trump) ya kujitoa katika makubaliano ya pande kadhaa hawezi kuwapiga faini wengine kutokana na kutekeleza makubaliano hayo. Lengo la Marekani kuhusiana na JCPOA ni kuyaangamiza kikamilifu makubaliano hayo. Hata hivyo pande zilizobakia zimeonyesha kwamba, kwa sasa zimechukua uamuzi wa kubakia katika makubaliano hayo na jambo hilo liliungwa mkono na Rais Hassan Rouhani alipofanya safari hivi karibuni huko Vienna.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Austria ameashiria nukta muhimu sana nayo ni kwamba, Marekani kama imejitoa katika makubaliano ya JCPOA kwa sababu yoyote ile inayoijua yenyewe, haina haki ya kuyalazimisha mataifa mengine yachukue uamuzi kama iliouchukua yenyewe. Pamoja na hayo, Bi Karin Kneissl hakubainisha sababu ya mwenendo huu wa Trump. Sababu ya hatua hiyo ya Trump ni sera za kibabe za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na za kuburi katika fremu ya nara ya "Marekani Kwanza" na wakati huo huo kupuuza maslahi ya mataifa mengine. Trump anaamini kwamba, utendaji wake huo utaiongezea nguvu Marekani na kuyashinda mataifa yanayoshindana na nchi hiyo.
Pamoja na hayo yote kinyume na matarajio ya Trump, utendaji wake huo haujawa na natija nyingine bighairi ya kutengwa nchi yake. Jean-Claude Juncker, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya anasema: Fikra ya Trump ya "Marekani Kwanza" au America First imepelekea Marekani ibaki peke yake.

Trump akiwa na lengo la kusukuma mbele gurudumu la siasa zake amekuwa akitumia mbinu ambazo hazijazoeleka ambazo ni kinyume na makubaliano ya jamii ya kimataifa na hata washirika wake wa Ulaya.
Licha ya kuwa Trump amezua mzozo mkubwa baina yake na madola ya Ulaya kuhusiana na masuala mbalimbali, lakini hitilafu kuhusiana na JCPOA zimekabiliwa na radiamali hasi na kali za madola ya Ulaya. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, Marekani ilijitoa katika makubaliano hayo bila ya sababu ya kimsingi licha ya Iran kuheshimu na kufungamana kikamilifu na makubaliano hayo.
Kabla ya hatua hiyo pia, matamshi na misimamo ya Trump ilikuwa imeleta anga hasi ya kisaikolojia dhidi ya kupanuka uhusiano wa kibiashara na kiuchumi wa nchi za Ulaya na Iran, lengo likiwa ni kuyakatisha tamaa na kuyafanya mashirika na taasisi za Ulaya ziondoke nchini Iran.

Licha ya msimamo huo wa Washington, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yana umuhimu mkubwa kwa Ulaya ambapo nchi hizo, kwa kutoa kifurushi cha mapendekezo kwa Iran, zinataka kuishajiisha Tehran ili iendelee kuheshimu makubaliano hayo.
Bi Karin Kneissl, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Austria anasema kuhusiana na hilo kwamba: Mada kuu ni kulinda makubaliano ya nyuklia na Iran, kwani kinyume na hivyo, makubaliano ya pande kadhaa yaliyosimama juu ya msingi wa kuaminiana yatakosa maana kabisa. Endapo JCPOA itasambaratika, kwa mtazamo wetu pia ni kuwa, misingi ya uhusiano wa kimataifa nayo itakuwa imesambaratika.
Kwa muktadha huo, kwa mtazamo wa Austria ikiwa nchi Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya ni kuwa, juhudi za kila upande za kuyalinda makubaliano ya nyuklia na Iran ya JCPOA zina umuhimu mkubwa na ni katika fremu ya kulinda maslahi ya muda mrefu ya kiusalama, kisiasa, kibiashara na kiuchumi ya umoja huo.