Dec 15, 2022 07:15 UTC
  • Zaidi ya 100 watiwa mbaroni Ufaransa katika hekaheka za ushindi wa soka dhidi ya Morocco

Polisi ya Ufaransa imetangaza kuwa zaidi ya watu mia moja wametiwa mbaroni mjini Paris baada ya timu ya soka ya nchi hiyo kuishinda Morocco katika nusu fainali ya Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar.

Furaha ya mashabiki wa Ufaransa baada ya ushindi wa timu yao dhidi ya Morocco katika nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022 imesababisha mapigano na polisi katika baadhi ya maeneo, na polisi imetangaza kukamatwa watu 115 katika mji mkuu Paris.
Kwa sababu ya kuhofia kutokea msongamano na mapigano, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa ilikuwa imetangaza tokea awali kuwa itasambaza askari polisi na askari wa ulinzi na ulinzi utaimarishwa zaidi nchini humo.
Katika miji ya Nice na Lyon katika mzunguko wa Belkor, kikundi cha vijana kiliwarushia fataki askari polisi na mapigano mengi yameripotiwa katika barabara ya Jean Madsen mjini Nice.
Baadhi ya watu katika eneo hilo walijaribu pia kuwashambulia mashabiki wa Morocco.
Askari usalama wa Ufaransa wakijaribu kudhibiti mashabiki wa soka

Polisi wa Lyon imetangaza kuwa, watu hao walikuwa wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Watu hao walijaribu kuwavamia wapita njia wenye asili ya Morocco na kutoa kauli mbiu dhidi yao.

Sherehe za kufurahia ushindi wa Ufaransa dhidi ya Morocco katika eneo la Montpellier pia ziliandamana na hali ya mivutano mikubwa. Vurumai na mapigano katika uwanja wa Comedy yalianza hata kabla ya mwamuzi kupuliza kipyenga cha kumalizika mechi hiyo.
Wakati wa sherehe hizo za ushindi wa Ufaransa dhidi ya Morocco, kijana mmoja Mfaransa mwenye asili ya Morocco aliuawa kwa kugongwa na gari huko Montpellier.
Jana usiku, ilifanyika mechi ya pili ya nusu fainali ya Kombe la Dunia la Qatar ambapo timu ya taifa ya soka ya Ufaransa iliweza kuishinda timu ya taifa ya soka ya Morocco kwa mabao 2-0 na kufanikiwa kuingia kwenye fainali ya mashindano hayo dhidi ya Argentina, itakayofanyika siku ya Jumapili.../

 

Tags