Jul 11, 2021 08:22 UTC
  • Kikao cha viongozi wa Ufaransa na kundi la nchi tano za Sahel

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ameonana na wakuu wa nchi tano za eneo la Sahel ya Afrika ambazo ni Chad, Mali, Burkina Faso, Mauritania na Niger. Ingawa kikao hicho kimefanyika kwa njia ya Intaneti, lakini Rais Mohammad Bazoum wa Niger yeye ameshiriki kikao hicho akiwa ziarani nchini Ufaransa.

Baada ya kikao hicho, Macron amewaambia waandishi wa habari kuwa, kwa muda sasa Ufaransa imekuwa na mpango wa kupunguza idadi ya wanajeshi wake katika eneo la Sahel barani Afrika.

Amesisitiza kuwa, katika nusu ya pili ya mwaka huu wa 2021, kambi za kijeshi za Ufaransa zitafungwa kaskazini mwa Mali na wanajeshi wa nchi hiyo watapelekwa kusini mwa Mali baada kupunguzwa idadi yao. Mwaka 2012, Mali ilishuhudia mapinduzi ya kijeshi, mapinduzi hayo yalitoa fursa kwa magenge ya kigaidi ambayo yametangaza waziwazi kuwa ni wafuasi wa mitandao ya kigaidi ya al Qaida na Daesh (ISIS) kushadidisha harakati zao kaskazini mwa Mali na kuteka maeneo mengi. Ufaransa ilitumia jambo hilo kama kisingizio cha kutuma wanajeshi wake huko Mali kwa madai ya kupambana na magaidi.

Licha ya Macron kutangaza uamuzi wa Ufaransa wa kufunga kambi za kijeshi za nchi hiyo huko kaskaizni mwa Mali, lakini mwenyewe amesema kuwa, Ufaransa itabakisha baina ya wanajeshi 2500 hadi 3000 katika eneo la Sahel kwa madai ya kutoa mafunzo ya kijeshi kwa askari wa wa vikosi maalumu vya serikali. Hivi sasa idadi ya askari wa Ufaransa walioko kwenye eneo la Sahel Afrika kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Paris, ni wanajeshi 5000.

Marais wa Niger na Ufaransa mjini Paris

 

Rais wa Ufaransa amesisitiza pia kuwa, licha ya kwamba Paris itapunguza idadi ya wanajeshi wake, lakini uwepo wake katika eneo la Sahel utaendelea kuwa mkubwa. Ufaransa inajifanya kwamba nchi za eneo la Sahel barani Afrika zinaihitajia mno Paris na haziwezi kuendelea na maisha yao bila ya kusimamiwa na kuendeshwa na mkoloni huyo kizee wa Ulaya. Hata hivyo madai hayo ya Paris yanasutwa na wataalamu wa mambo.

Abdul Wahid Olad Mauloud, mtafiti wa Morocco ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya usalama katika eneo la Sahel anasema, si jambo la kushangaza hata kidogo kuona Paris inang'ang'ania kubakia wanajeshi wake katika nchi kama Mali kwani Ufaransa ni mkoloni wa jadi na dhati yake ni kuzikoloni nchi za Afrika katika kila kitu. Paris haiko tayari kuona inalipoteza eneo la Sahel kwa gharama yoyote ile.

Mwezi uliopita pia, yaani tarehe 19 Juni, Macron alisema mbele ya waandishi wa habari kabla ya kuanza kikao cha viongozi wa kundi la G7 kwamba sehemu kubwa ya wanajeshi wa Ufaransa wataondoka katika eneo la Sahel la barani Arika. Kwa miaka minane sasa Ufaransa imetuma wanajeshi wake kwenye eneo hilo kwa madai ya kusaidia askari wa kieneo kupambana na magaidi kama wa al Qaida na Daesh (ISIS).

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron

 

Dalili zinaonekana wazi kwamba, Ufaransa haikutuma wanajeshi wake katika eneo la Sahel Afrika kwa ajili ya kuondoka, bali ni kwa ajili ya kubakia muda mrefu au hata milele. Sasa hivi inadai kuwa imekusudia kupunguza idadi ya wanajeshi wake kwenye eneo hilo, lakini wakati huo huo inasisitiza kuwa, itahakikisha uwepo wa Paris katika eneo la Sahel Afrika unakuwa mkubwa zaidi na zaidi.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kuna mambo kadhaa ambayo yamepelekea sasa hivi Ufaransa izungumzie suala la kupunguza wanajeshi wake barani Afrika. Ingawa Paris inadai kuwa hatari katika eneo hilo zimepungua, lakini wachambuzi wa mambo wanasema, uwepo wa miaka mingi wa wanajeshi wa Ufaransa katika eneo la Sahel Afrika haujazaa matunda yoyote ya maana zaidi ya kuongezeka tu mashambulizi na vitendo vya kigaidi. Magenge ya kigaidi yanatumia kisingizio hicho hicho cha kupambana na madola ya kigeni, kuvutia wafuasi wengi zaidi hasa vijana. Sababu nyingine ni kwamba, Ufaransa haitaki kubeba peke yake jukumu la kupambana na ugaidi katika eneo hilo. Sasa kwa madai ya kupunguza idadi ya wanajeshi wake, Paris inataka kuziambia nchi nyingine kuwa nazo zinapaswa kuungana nayo katika hicho kinachodaiwa ni vita dhidi ya ugaidi katika eneo la Sahel Afrika.

Tags