Oct 19, 2023 10:50 UTC
  • Kikao kisichokuwa na natija cha Baraza la Usalama: Marekani yapinga usitishaji mapigano Gaza

Jumatano, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikataa tena azimio la kusitisha mapigano huko Gaza kufuatia upinzani wa Marekani. Marekani ilipinga azimio lililopendekezwa kwa Baraza la Usalama na Brazil, lililotaka kusitishwa mapigano ili kufikishwa misaada ya kibinadamu Ghaza.

 

Azimio hili lilikuwa na kura 12 za ndio, na nchi mbili za Uingereza na Russia hazikupiga kura. Azimio hilo lililopendekezwa na Brazil, halikuashiria  utawala wa Kizayuni kulenga  maeneo ya umma, hospitali na shule katika mashambulizi yake, hivyo, Russia ikajiepusha kuliunga mkono. Marekani ilitumia haki yake ya kura ya turufu kulipinga azimio hilo. Kwa hivyo, azimio hilo halikupitishwa, na kiutendaji, kikao cha Baraza la Usalama kikamalizika bila natija yoyote.

Kura ya turufu ya Marekani dhidi ya Azimio la Baraza la Usalama kuhusu Ghaza imekabiliwa tena na radiamali kali kutoka kwa mataifa mawili ya kimataifa washindani wa nchi hiyo, yaani Russia na China.

Russia ilisema kupitia taarifa ya kukosoa vikali hatua hiyo ya Marekani: Barakoa zimeondolewa.

Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa, Vasily Nebenzia, alisema: Russia inasikitishwa na suala kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepoteza fursa kwa kutopitisha azimio la Moscow kuhusu Ghaza siku ya Jumatatu, na kupelekea watu zaidi kuuawa.

Zhang Jun, Mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa pia amesema: Kura ya turufu ya Marekani dhidi ya azimio lililopendekezwa na Brazil kwa ajili ya kusitishwa mzozo kati ya utawala wa Israel na Hamas katika Baraza la Usalama haikubaliki.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Awali Marekani na waitifaki wake wa Magharibi walilipinga azimio lililopendekezwa na Russia la usitishaji vita huko Ghaza siku ya Jumatatu, na hivyo kuuwandalia utawala wa Kizayuni uwanja wa kuendelea kuishambulia Ghaza na kuwaua wananchi wasiokuwa na hatia wa Palestina. Nchi hzi hizo zilidai kuwa hazitapiga kura kwa azimio lililopendekezwa na Russia kutokana na kuwa halikuunga mkono haki ya kujilinda utawala wa Kizayuni na Hamas haikulaaniwa kwa mashambulizi yake.

Nukta muhimu ni kwamba Marekani, Uingereza na Ufaransa, zikiwa Wanachama wa Kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoka muungano wa Magharibi, ziliazimia kutopitisha azimio la kusitishwa mashambulizi dhidi ya Ghaza kwa kuzingatia uungaji mkono wao wa pande zote kwa utawala wa Kizayuni. Wakati huo huo, nchi hizo hazipendekezi azimio au kutoa pendekezo lolote la usitishaji vita ua kusimamisha mashambulizi ya utawala wa Kizayuni, na hata katika kikao cha Jumatano hazikuwa tayari kuchukua hatua yoyote katika uwanja huo. Riyad Mansour, Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa alisema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba baraza hilo limeshindwa kuchukua hatua zozote ili kusimamisha mauaji ya kinyama yanayofanywa na Utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina.

Hayo yanajiri licha ya kwamba mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza yameongezeka katika siku za hivi karibuni. Katika kukabiliana na kufedheheshwa kwake kijeshi, kiusalama na kijasusi na wanamuqawama wa Palestina katika operesheni ya Kimbunga cha ya Al-Aqsa, Tel Aviv imelenga miundombinu muhimu ya makazi ya Ukanda wa Ghaza kwa mashambulizi yake ya kinyama. Jumanne jioni, Utawala wa Kizayuni ulilenga kwa makusudi hospitali ya Kibaptisti huko Ghaza katika jinai ya kivita, na kwa mujibu wa ripoti, takriban watu 1000 ambao wengi wao walikuwa watoto na wanawake waliuawa shahidi.

Maafa ya Ghaza

Wakati huo huo licha ya jinai kubwa mno zinazofanywa na utawala wa Kizayuni, lakini katika safari yake ya karibuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina Rais Joe Biden wa Marekani amesisitiza juu ya kuendelea kuongeza misaada yake ya kijeshi kwa Tel Aviv.

Katika siku za hivi karibuni,  Biden amekuwa akikariri ahadi na uungaji mkono wa nchi yake kwa utawala wa Kizayuni licha ya kushambuliwa kwa mabomu Ukanda wa Ghaza na kusema kuwa, misaada hiyo kwa Israel ina uungaji mkono mkubwa wa mirengo yote miwili ya kisiasa katika bunge la Marekani. Ameongeza kuwa anatathmini kifurushi kipya cha msaada wa kijeshi cha dola bilioni 100 cha nchi hiyo kwa Israel na Ukraine. Iwapo Bunge la Congress litaidhinisha msaada huo wa kijeshi kwa Israel, utawala huo utakuwa mpokeaji wa pili mkubwa wa msaada wa kijeshi wa Marekani. Taarifa zilizochapishwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani zinaonyesha kuwa Israel ilipokea msaada wa zaidi ya dola bilioni 63 kuanzia mwaka 2001 hadi 2023.

Tags